Isaiah 26

Wimbo Wa Ushindi

1 aKatika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda: Tuna mji ulio na nguvu,
Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake.

2 bFungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia,
taifa lile lidumishalo imani.

3 cUtamlinda katika amani kamilifu
yeye ambaye moyo wake ni thabiti
kwa sababu anakutumaini wewe.

4 dMtumaini Bwana milele,
kwa kuwa Bwana, Bwana, ni Mwamba wa milele.

5 eHuwashusha wale wajikwezao,
huushusha chini mji wenye kiburi,
huushusha hadi ardhini
na kuutupa chini mavumbini.

6 fMiguu huukanyaga chini,
miguu ya hao walioonewa,
hatua za hao maskini.


7 gMapito ya wenye haki yamenyooka.
Ewe uliye Mwenye Haki,
waisawazisha njia ya mtu mnyofu.

8 hNaam, Bwana, tukienenda katika sheria zako,
twakungojea wewe,
jina lako na sifa zako
ndizo shauku za mioyo yetu.

9 iNafsi yangu yakutamani wakati wa usiku,
wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku.
Wakati hukumu zako zinapokuja juu ya dunia,
watu wa ulimwengu hujifunza haki.

10 jIngawa neema yaonyeshwa kwa waovu,
hawajifunzi haki,
hata katika nchi ya unyofu huendelea kutenda mabaya
wala hawazingatii utukufu wa Bwana.

11 kEe Bwana, mkono wako umeinuliwa juu,
lakini hawauoni.
Wao na waone wivu wako kwa ajili ya watu wako tena waaibishwe,
moto uliowekwa akiba kwa ajili ya adui zako na uwateketeze.


12 l Bwana, unaamuru amani kwa ajili yetu,
yale yote tuliyoweza kuyakamilisha ni wewe uliyetenda kwa ajili yetu.

13 mEe Bwana, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametutawala,
lakini jina lako pekee ndilo tunaloliheshimu.

14 nWao sasa wamekufa, wala hawako tena hai,
roho za waliokufa hazitarudi tena.
Uliwaadhibu na kuwaangamiza,
umefuta kumbukumbu lao lote.

15 oUmeliongeza hilo taifa, Ee Bwana,
umeliongeza hilo taifa.
Umejipatia utukufu kwa ajili yako mwenyewe,
umepanua mipaka yote ya nchi.


16 p Bwana, walikujia katika taabu yao,
wewe ulipowarudi,
waliweza kuomba kwa kunong’ona tu.

17 qKama mwanamke mwenye mimba aliyekaribia kuzaa
anavyogaagaa na kulia kwa ajili ya maumivu yake,
ndivyo tulivyokuwa mbele zako, Ee Bwana.

18 rTulikuwa na mimba, tuligaagaa kwa maumivu,
lakini tulizaa upepo.
Hatukuleta wokovu duniani,
hatujazaa watu katika ulimwengu huu.


19 sLakini wafu wenu wataishi,
nayo miili yao itafufuka.
Ninyi mnaokaa katika mavumbi,
amkeni mkapige kelele kwa furaha.
Umande wenu ni kama umande wa asubuhi,
dunia itawazaa wafu wake.


20 tNendeni, watu wangu, ingieni vyumbani mwenu
na mfunge milango nyuma yenu,
jificheni kwa kitambo kidogo
mpaka ghadhabu yake ipite.

21 uTazama, Bwana anakuja kutoka makao yake
ili kuwaadhibu watu wa dunia kwa ajili ya dhambi zao.
Dunia itadhihirisha umwagaji damu juu yake,
wala haitaendelea kuwaficha watu wake waliouawa.
Copyright information for SwhKC